UJUE UMUHIMU WA KUIOMBEA NAFSI YAKO
UJUE UMUHIMU WA KUOMBEA NAFSI YAKO.
Zaburi:42.2-6 Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu. Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu. Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.
Bwana Yesu asifiwe sana sana.
Biblia inatueleza kuwa Nafsi ni uhai; kwenye;
Mwanzo:2.7
Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.
Na ukisoma kwenye 42:2 utaona neno likisema hivi; "Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU,Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?"
Maana yake ni kwamba uhusiano kati ya mtu yaani mwili na roho ya mtu na Roho ya Mungu unategemea sana uwepo wa nafsi iliyo hai.
Pasipo nafsi mwili wa mtu hauna kazi, haufai kwa lolote mbele za Mungu ,pia na roho ya mtu inakuwa haina maana ndani ya mwili wa mtu wala haifai kitu kabisa, nafsi ndiyo inayotia uzito wa kuwepo kwa mwili na roho sehemu moja na kushirikiana kwa pamoja, na pia ndiyo lango au mlango wa kupitia Roho ya Mungu kuja kwenye mwili na roho ya mtu ,kufanya kazi yake inayokuwa ikitaka kuifanya.
Ndio maana mwandishi wa Zaburi ya 42:2, anasema "Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU.."
Maana yake ni kwamba kwenye nafsi yake kuna chemchemi au chanzo cha shauku ya kumtaka au kumtafuta Mungu aliye hai na nafsi yake ndiyo yenye kuhinua ile shauku, ndiyo yenye kuhitazamia ile shauku ,kwamba ni Lini sasa itaenda kutimizwa ndani yake.
Ili upate kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wako ,nafsi yako inatakiwa ikae sawa sawa, isipokaa sawa au vizuri, ujue uhusiano wako na Mungu hautakuwa mzuri, utakuwa na shida tu daima.
Ukisoma neno la Mungu kwenye Wagalatia:2.20,utaona linasema; "Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu."
Mwanzo 2:7 inatueleza kwamba nafsi ni uhai ulioko ndani ya mwili huu wa damu na mwili lakini Wagalatia 2:20 inatueleza juu ya kuwepo kwa aina mpya ya uhai na aina hiyo ya uhai na yenyewe inaweza kuingizwa ndani ya mwili wa mwanadamu.
Na kinachoshangaza zaidi ni hiki ,ni kule kuona jinsi Mungu anavyoutazama uhai au nafsi kama sehemu au eneo la Muhimu kwake la kuachilia mambo yake kwa mwanadamu.
Mungu ni Roho maandiko yanatueleza kuwa pale mwanzoni alimpulizia mwanadamu uhai wake akawa nafsi hai lakini Wagalatia 2:20 inatueleza kuwa Mungu amerudia tena tendo la kuachilia uhai wake ndani ya mwanadamu ,lakini safari hii ,ametupa heshima zaidi ,ametupa uhai ule ulioko ndani ya Mwanae mpendwa yaani Yesu Kristo, ametupa nafsi ya Mwanae ndani yetu, ili kusudi tupate kuwa sehemu ya uungu wake na washirika wakamilifu wa tabia , nguvu na maisha yake ya uungu oooh Glory glory kwa Mungu wetu.
Sasa sikia hapa pana siri nzito mno, ukifanikiwa kunasa hii siri, kuna mambo utaanza kuyaona na kuyagundua ya ajabu sana sana.
Sikia ,kumbe uhai unaweza kutolewa kutoka mahali fulani na ukaingizwa sehemu nyingine na ukafanya kazi mahala ulipoweka ,na ile kazi ikawa ni ya kufanana na kusudi au nia ya mtoa uhai huo ilivyo.
Nafsi au uhai unaweza kuchukuliwa au kutekwa na kupelekwa sehemu nyingine na pia uhai au nafsi inaweza kuingiziwa uhai au nafsi nyingine na ikasababisha maisha kubadilika kabisa.
Wakati fulani nilikuwa naongea na mtu ambaye alikuwa akiota akijiliwa na watu wa familia yake waliokufa na nikamwelezea kuwa kuna roho za wafu zinakufuatilia kwa makusudi yao maovu kwako na nikamwambie twende tuombe, tukiwa tunaomba ghafla akaanza kutoa pumzi nje kwa kasi ,puani na mdomoni na akaendelea kwa muda kidogo na ghafla katikati ya lile zoezi la utoaji wa pumzi ile ,sauti ikasikika ya mtu ikisema tuko ndani yake humu kwa muda mrefu sana sana, wewe ni nani unayetusumbua, sisi ni wazee wa familia yake, huyu tulipewa ,ni wa kwetu;maana yake ni kwamba alikuwa anaishi na uhai wake ulikuwa umefichwa au umeshikiliwa na uhai mwingine wa roho za familia, na kilichokuwa kikileta aina ya maisha aliyokuwa akiyaishi si Roho ya Mungu ,wala si roho yake bali ni roho za wafu ambazo zilikuwa zikitumia uhai waliokuwa wamemwingizia ndani yake ,ndani ya mwili wake na ndio maana wakati wa maombi alikuwa akipumua na kutoa ule uhai nje kwa nguvu.
Sikia mtu wa Mungu, kumbe unaweza ukawa unaishi kabisa lakini uishi kwa nafsi au uhai wako, unaishi kwa nafsi au uhai wa roho ya familia ambao ile roho ya familia imeupachika au kukupandikizia juu ya uhai wako kwa ajili ya kufanikisha mambo yao, au malengo na makusudi yao katika maisha yako.
Ndio maana Wagalatia 2:20 inatufunulia siri kwamba Kristo Yesu aliyekufa na kisha kufufuka anaweza leo kabisa akapewa nafasi nafsini au kwenye uhai wa mtu na akaingia na kuyamiliki maisha ya mwanadamu kikamilifu na kumbadilisha akawa ni kiumbe kipya, hii ni habari njema kwetu leo, kwamba Kristo mfufuka anaweza kuingia ndani yetu na kutufanya wana wa Mungu, warithi na washirika wakamilifu wa mambo ya kiungu ooh haleluya haleluya, Kristo ni tumaini la kuurithi uzima wa milele, ukimwamini leo, atakuokoa na kukufungua kutoka kwenye vifungo vilivyofunga nafsi au uhai wako na kukuzuia kuyaishi mapenzi na makusudi ya Mungu katika maisha yako.
Comments
Post a Comment