JE UNAJUA NINI CHA KUFANYA JUU YA MADHABAHU YA GIZA
JE UNAJUA NINI CHA KUFANYE JUU YA MADHABAHU YA GIZA?
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna aina mbili za madhabahu.
Kuna madhabahu ya MUNGU na kuna madhabahu ya shetani.
Madhabahu ni katikati ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Madhabahuni ni mahali ambapo vitu kutoka ulimwengu wa roho vinapitia kabla ya kuja katika ulimwengu wa mwili.
Madhabahu ya ki MUNGU hupitisha Neno la MUNGU na mambo ya ki MUNGU yote.
Madhabahu ya shetani ndio kiwanda cha kuleta matatizo katika maisha yako.
Madhabahu ya kishetani ambayo ndio madhabahu ya giza huleta laana, magonjwa, vifungo, mikosi, balaa na kila maroho ya kuzimu.
Ukitaka kuyashinda kila mashambulizi yanayotoka kwa mawakala wa shetani kuja kwako basi usisahau kuomba maombi ya kuvunja na kubomoa madhabahu za giza zinazotengeneza mabaya kuja kwako.
Sasa kwa sababu kuna aina mbili za madhabahu niko hapa Leo kukuonya kwamba usihusike kivyovyote na madhabahu ya shetani.
Kumbuka neno hilo na usije ukasahau kamwe kwamba madhabahu ya kishetani ipo tu kwa ajili ya uharibifu kwa wanadamu.
Yohana 10:10a ''Mwivi(shetani) haji ila aibe na kuchinja na kuharibu;''
Ukitaka connection na kuzimu basi fanyia kazi maelekezo ya madhabahu za kishetani, ukitaka uingie kwenye barabara pana ila ni ya kukupeleka jehanamu basi jiambatanishe na madhabahu ya kishetani.
Madhabahu ya kishetani ndio madhabahu za Giza, ndio madhabahu za kuzimu, hiyo haitakiwi kuhusika na wewe mwanadamu uliyeumbwa na MUNGU.
MUNGU anawataka watu wake walio Kanisa hai kwamba wahakikishe wanavunja madhabahu za giza na kuharibu kila kitu kinachohusika na shetani.
Kumbukumbu 12:3 ''nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo. ''
Unapokwenda kwa mganga wa kienyeji ujue unaifuata madhabahu ya kishetani.
Unapokwenda kutambika ujue unaifuata madhabahu ya kishetani na uharibifu wako.
Unapokuwa mchawi au mganga wa kienyeji au sangoma au mnajimu unakuwa mtenda kazi wa madhabahu ya kishetani.
Unapoingia agano lolote la kishetani ujue unamkaribisha shetani maishani mwako, na yeye akija ni kwa ajili ya uharibifu wako na kuhakikisha huendi uzima wa milele.
Unapoingia mikataba ya kishetani au unapoingizwa kwa siri katika mikataba ya kishetani inakupasa kuvunja haraka sana mikataba hiyo kwa wewe kumkimbilia YESU KRISTO Mwokozi anayeokoa.
Ndugu usikubali kuhusika na madhabahu za kipepo kwa namna yeyote.
Kutoka 34:12-15 ''Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.
Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao. Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni MUNGU mwenye wivu. Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake. ''
Kama ulitoa sadaka kwenye madhabahu za kishetani tambua kwamba sadaka yako hiyo ndio ilikuwa muhuri wa agano la kipepo la kukufunga wewe.
Sadaka ina nguvu sana lakini ukiitoa katika madhabahu ya MUNGU na sio ya shetani.
Madhabahu ya MUNGU ipo katika KRISTO YESU pekee.
Ndugu usikubali kuhusika na madhabahu ya kishetani kwa namna yeyote ile.
Madhabahu sahihi unayotakiwa kuhusika nayo ni madhabahu ambayo watu wa hapo wameokoka na YESU KRISTO ni Bwana na Mwokozi wao.
Husika kumpa sadaka au zaka au shukrani au malimbuko Mtumishi wa KRISTO aliye mwaminifu na Mtumishi huyo lazima awe ameokolewa na YESU KRISTO Mwokozi.
Kumb 12:13-14 ''Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; bali katika mahali atakapopachagua BWANA katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.''
Nakuomba usihusike kwa namna yeyote ile na madhabahu ya kishetani maana hiyo ipo kwa ajili ya uharibifu wako tu.
Husika daima na madhabahu ya MUNGU aliye hai.
Madhabahu ya MUNGU inahusika na mambo makuu yafuatayo;
1. Kumwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli.
Yohana 4:24 ''Mungu ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.''
2. Wokovu wa YESU KRISTO.
Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''
3. Kuongozwa na kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
Hiyo ndio madhabahu safi ya kiroho.
Lakini pia madhabahu bila sadaka haiwi madhabahu kamili.
Katika maandiko mengi zaidi ndani ya Biblia ilipotajwa madhabahu na matoleo yalitajwa hivyo kiroho matoleo safi na ibada safi huikamilisha madhabahu safi.
Mfano ni huu Mwanzo 8:20 '' Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. ''
Penda sana kutoa matoleo yako katika madhabahu ya MUNGU aliye hai.
Kwenye ufalme wa giza wao wanajua sana nguvu za sadaka ndio maana huko sadaka/kafara ni jambo la lazima.
Hivyo ifute nguvu ya sadaka zao kwa maombi na huku ukimtolea MUNGU aliye hai sadaka.
Nini ufanye kuhusu madhabahu za Giza?
1. Omba maombi kupitia jina la YESU KRISTO na damu ya YESU KRISTO ukivunja madhabahu hizo za giza ili zisilete tena uharibifu kwako.
Kumb 7:5 ''Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''
2. Wapige kwa moto wa MUNGU makuhani wa madhabahu za Giza pamoja na watenda kazi wa hiyo madhabahu ya giza.
Zaburi 71:13 '' Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.''
3. Futa kwa damu ya YESU kila sadaka/kafara ya agano iliyofanyika kwenye madhabahu za giza kukuhusu wewe.
Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; .......''
4. Futa uchawi na sumu za kichawi zilizokupata zinazotokana na madhabahu za giza.
Kutoka 22:18 '' Usimwache mwanamke mchawi kuishi.''
5. Mpinge mungu wa madhabahu hizo za giza naye atakukimbia hakika.
Yakobo 4:7b ''Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. ''
6. Omba kwa MUNGU kwamba YESU KRISTO kupitia ROHO MTAKATIFU amiliki na kutawala roho yako, nafsi yako na mwili wako. Ndipo kuanzia hapo madhara kutoka madhabahu ya unayoshindana nayo hayatakugusa.
1 Yohana 4:4 ''Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. ''
7. Kubwa kuliko yote katika maombi yako omba mkono wa MUNGU wa kuangamiza unyoshwe kwenye madhabahu za Giza zilizokuwa zinakutesa.
Kumb 2:15 ''Tena mkono wa BWANA ulikuwa juu yao ili kuwaangamiza, kuwatoa kati ya marago, hata walipokoma.''
Ufunuo huu kuhusu mkono wa MUNGU niliupata siku za karibuni tu na hakika ukijua kuomba kwa kumuomba MUNGU kwamba mkono wake ufanye kazi hakika ushindi wake ni mkubwa sana sana.
8. Mshukuru MUNGU kwa maombi yako na nakuomba uwe mtu wa kuijenga madhabahu ya MUNGU na sio kuibomoa.
Zaburi136:2-3 ''Mshukuruni MUNGU wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni BWANA wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele. ''
Pia anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana, ili madhabahu za Giza zikose tena uhalali wa kukuonea, tena husika kuijenga madhabahu ya MUNGU katika KRISTO YESU.
Mwanzo 35:3 " Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia MUNGU madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea."
Madhabahu ya MUNGU Kanisani kwenu hakikisha inafanya kazi ili mungu wa madhabahu nyingine asiingilie madhabahu ya MUNGU Kanisani kwenu.
Wewe kama mteule wa KRISTO uko katika madhabahu ya MUNGU aliye hai, hakikisha madhabahu hiyo inafanya kazi siku zote ili mungu wa madhabahu nyingine asivamie madhabahu hiyo na kuiondoa kutoka madhabahu ya MUNGU na inakuwa madhabahu ya mungu yaani ya kishetani.
Madhabahu ya MUNGU Kanisani kwenu inapokuwa inafanya kazi itamruhusu MUNGU kuihudumia, itamruhusu Bwana YESU kuihudumia na itamruhusu ROHO MTAKATIFU kuihudumia.
Usiruhusu mafundisho ya uongo katika madhabahu ya MUNGU Kanisani kwenu.
Usiruhusu mafunuo ya kishetani kufanya kazi katika kanisa Leo.
Usiruhusu ukweli wa Neno la MUNGU upindishwe Kanisani kwenu.
Mkifanya hivyo ujue mtasababisha MUNGU katika KRISTO YESU kwa njia ya ROHO MTAKATIFU asiwahudumie.
Hakikisha madhabahu ya MUNGU iliyo kwenu haivamiwi na mawakala wa shetani.
Hakikisha madhabahu ya MUNGU kwenu inaambatana na Neno la MUNGU na nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Zaburi 43:4 "Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa MUNGU, kwa MUNGU aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, MUNGU wangu."
Madhabahu ni kituo kutolea taarifa kutoka ulimwengu wa roho kuja ulimwengu wa mwili.
Unapaswa sana kuiheshimu madhabahu ya MUNGU aliye hai katika KRISTO YESU.
Hakikisha unazingatia maagizo ya MUNGU kutoka katika madhabahu yake.
Mtumishi wa KRISTO yeyote mwaminifu ni mtenda kazi katika madhabahu ya MUNGU.
Inakupasa sana kuilinda madhabahu ya MUNGU ili isivamiwe na mawakala wa shetani.
Uwe makini sana na mwangalifu ili usiwe sehemu ya kuibomoa madhabahu ya MUNGU katika KRISTO YESU.
Hakikisha unailinda madhabahu ya MUNGU.
Isaya 56:7 " Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote."
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255756717689
(Hadi whatsapp).
+255788717689
makubimsafiri@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Comments
Post a Comment