HISTORIA YAKO ISIKUHUKUMU.

HISTORIA YAKO ISIKUHUKUMU.

"  Ilikuwa ni mida ya saa moja usiku, ninajiandaa kwenda Kwenye harusi. Nikapigiwa simu kwamba hakuna harusi, kwa sababu jana bwana harusi alipata cv ya mchumba wake, akathibitisha kuwa yule mchumba hakuwa na historia nzuri.

Ni wengi wamekataliwa sababu za historia zao. Jana pia nilipokea simu inayotaka nithibitishe historia ya kijana niliyefanya nae kazi miaka 8 iliyopita. Wakaniambia ameandika alifanya hapo kazi, tafadhali tuambie iwapo ni mtu mwema, ili tumthibitishe kazini. Hii ina maana mbili, kwamba wapo wanaokubalika kwa sababu ya historia na wapo wanaokataliwa kwa sababu ya historia.

Leo nataka niongee na wewe uliyekataliwa kwa sababu ya historia. Mtume Paulo alikuwa ni muuaji, lakini Mungu akambadilisha kuwa ni  mtumishi wake. Gideon alikuwa muoga aliyekosa ujasiri lakini Mungu  alimbadilisha kuwa jasiri. Moses alikuwa muuaji lakini Mungu alimbadilisha kuwa kiongozi, Yusufu alikuwa mtumwa, lakini Mungu alimbadilisha kuwa kiongozi. 

Ni kweli kabisa, nakubali na naafiki yeyote anayehoji historia lakini naamini na nimeshuhudia katika maisha yangu kwamba mwenye uwezo wa kumbadilisha mtu sio mimi wala wewe, sio pesa wala elimu ni Mungu mwenyewe.

Miaka michache iliyopita, nilipoteza kazi na matumaini, nilipoteza marafiki na watu wa kuniunga mkono lakini nilipigana nisimpoteze Mungu, nisitende dhambi wala nisiharibu hekalu lake ndani yangu, na Mungu huyo huyo alinisimamia, akanibadilisha, yote yale pamoja na machungu yake na maumivi yake yakawa historia, yaliyobaki ni makovu yanayokauka taratibu.

Unaweza ukafikiri waliobadilishwa ni waliokuwepo kwenye  biblia, ngoja nikuambie kitu, hata leo hii unaweza kubadilishwa. Haijalishi umekataliwa na wanaume wangapi au mabinti wangapi kwa sababu historia yako ni chafu. Hao ni binadamu, usipambane wakukubali siri ya kubadilika na kukubaliwa haiko kwao wewe usikate tamaa, matumaini yako mpe Mungu wako.

Hapa karibuni nilikuwa naongea na rafiki yangu mmoja ofisini kwangu. Akaniambia Mrisho, sisi binadamu tuna tabia asilia, hata rafiki yako wa karibu akisikia umepoteza cheo au kazi au pesa hata  mtazamo wake kwako unabadikika. (Nikamwambia binafsi niliyaona haya nilipo pangiwa kazi nyingine nilipotoka kuwa Dc Korogwe). Hata  akiona simu yako  anachukua dakika kufikiri iwapo aipokee au asiipokee. Wakati enzi ya ufalme wako hata angekuwa anaoga angetoka bila taulo kupokea simu yako.

Mimi nilimuelewa sana Magreth. Ndio sababu leo nataka ufikirie tofauti, wala uwepo wako hapa duniani usiwekwe dhamana kwa mali, pesa na vyeo, kwa maana pesa na vyeo vinaweza vikaondoka wakati wowote, lakini kile alichoweka Mungu ndani yako hakiwezi kuondoka. Leo mimi Mrisho naandika kwa sababu kuna kitu Mungu ameweka ndani yangu, kwa sababu nimepitia mitihani na Majaribu ya maisha yangu ni Somo kwa wengine.

Usikate tamaa kwa sababu ulikuwa na historia ya pesa leo huna. Kwa sababu una miaka KADHAA  toka umalize Shule Lakini hadi leo huna kazi. Kwa sababu ulifukuzwa kazi kwa kuonewa. Kwa sababu hata kinachosemwa kwako ni historia! Angalia ulichonacho ndani yako, hicho ndicho kiletacho vyote vionekanavyo kwa macho. Tumaini lako mpe Mungu wako, yeye alimbadilisha Sauli kuwa Paulo, anaweza akambadilisha masikini kuwa tajiri na mtumwa kuwa mfalme.

Comments

Popular posts from this blog

NINI MAANA YA NAFSI, ROHO, MOYO NA MWILI.?

USHUHUDA WA ALIEKUWA WAKALA WA SHETANI

BWANA YU PAMOJA NAWE EE SHUJAA