USIPOBARIKIWA MJINI UTABARIKIWA MASHAMBANI
USIPOBARIKIWA MJINI UTABARIKIWA MASHAMBANI
Jina la Bwana wetu YESU KRISTO litukuzwe mpendwa wangu Karibu tujifunze Neno la MUNGU,
Natamani somo hili liwafikie watu wengi zaidi wasome somo hili kuanzia mwanzo hadi mwisho, maana kuna kitu chake cha pekee ROHO MTAKATIFU amemuandalia kila mtu kupitia somo hili la ufunuo wa Mungu mwenyewe.
Usipopata baraka mjini hamia mashambani utabarikiwa iko kwenye Biblia hii,
Inawezekana likawa Neno gumu sana kwako ila nisikilize itakusaidia ili utoke na kitu usibaki kama ulivyo fungua akili yako kupokea kitu kipya.
Kumbukumbu la torati 28:3 Utabarikiwa mjini, tabarikiwa na mashambani.
Maana yake MUNGU anaweza kuachilia baraka popote iwe ni mjini au vijijini kwenye mashamba, Maana yake ukiona jambo moja limeshindikana kukuletea baraka unayo itarajia sio dhambi kuhamia jambo lingine. mfano kama biashara yako haikulipi hamia kwenye Kilimo, Kama kilimo hakikulipi hamia ufugaji, Kama ajira haikulipi basi jiajiri mwenyewe, baraka za MUNGU hazijaachiliwa katika eneo moja tu bali zimeachiliwa maeneo mengi sana tena tofauti tofauti, Mradi ni unafanya kazi halali mbele za MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi, na njia mojawapo ya kufanikiwa kama wewe ni muombaji basi ni kumsikiliza ROHO MTAKATIFU anakupa amani katika jambo gani la kufanikiwa kwako na ulifanye kwa bidii sana kwa moyo wote kwa kujituma mno,
Sina maana kwamba lazima ukaishi vijijini ila nina maana kwamba baraka za MUNGU ziko katika maeneo mengi maana wako watu wanaishi mjini lkn ni wakulima na wengine ni wafugaji, sio eneo moja tu.
Kama sio ofisini kuna kilimo, kama sio kilimo kuna biashara, MUNGU anaposema kwamba atakubariki mjini na atakubariki mashambani ina maana ya kwamba baraka za MUNGU zimeachiliwa maeneo mengi sio eneo moja tu.
Kumbuka pia ROHO MTAKATIFU na anakusaidie kuliendea eneo ambalo utakuwa salama, utakuwa na muda wa kumwabudu MUNGU Baba, utakuwa na muda wa kumtumikia Bwana YESU KRISTO na utakuwa na mafanikio ya kiroho na kimwili maana vyote hivi vyahitajika katika maisha ya mwanadamu.
Kumbukumbu la torati 28:8 "BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako."
MUNGU anaweza kuiamuru baraka ije kwako haijalishi uko wapi au uko katika ardhi ya eneo gani maana imeandikwa atazitikisa mbingu na anga na kukunyeshea mvua ya baraka.
Andiko li kumbukumbu la torati 28:8 lina maana pia kwamba "MUNGU atakubarikia katika ardhi akupayo" hivyo husika na maombi ya kuombea ardhi unayoishi, Mawakala wa shetani wakati mwingine huifunga ardhi kipepo hivyo kama unaishi juu ya ardhi hiyo huwezi kufanikiwa,
Unaweza kuwa mjini na umefungua duka, na ardhi ya eneo hilo imefungwa kishetani na mawakala wa shetani, usipoiombea ardhi hiyo na kuikomboa kwa damu ya YESU KRISTO ujue utasumbuka sana kufanikiwa na ukweli hautafanikiwa kamwe,
Unapoombea baraka zako kumbuka sana kuombea ardhi ya eneo lako la kazi ndipo utaiona baraka yako,
Pamiliki hapo kwenye ulimwengu wa roho ili adui asipafunge ili wewe usifanikiwe na uwe nyota ung'ae,
Kumbukumbu la torati 11:24 "Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, la Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu."
Kila mtakapopakanyaga patakuwa penu maana yake mtamzuia adui kupafunga hapo wala kupateka maana mmepewa utawala na kumiliki, Inawezekana wewe unafanya kazi ofisi Fulani na ardhi ya hapo imefungwa kipepo na adui, ndio maana hufanikiwa, Inawezekana wewe unalima katika ardhi iliyofungwa, Inawezekana wewe unaishi katika ardhi iliyofungwa, Kumbuka mafanikio yako yote yanategemea wewe mwenyewe haijalishi upo wapi ila hayo mafanikio yanategemea ardhi iwe kwa ofisi, biashara, kilimo, usafirishaji, uchuuzi n.k
Kumbuka tu baraka zako ziambatane na kufanya kazi halali, kisha uwe mtoaji wa fungu la kumi kwa uaminifu na ikumbukwe fungu la kumi hutolewa mahali ambapo unasali/unaabudu na sio sehemu nyingine pia uwe muombaji na unayeishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.
NINI UFANYE KWENYE MAOMBI?
1. Tubu kwa ajili ya ardhi ya eneo lako la kazi hili ni jambo muhimu sana na la kwanza kwa mafanikio yako.
2Nyakati 7:14" ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao."
Kuiponya nchi yao maana yake kuiponya ardhi yao nchi inapo ponywa kila kitu kinakuwa Sawa wanyama ndege mimea vyote vinamtegemea mwanadamu ili viwe salama na shetani asivishambulie ni jukumu lako kuiombea ardhi yako.
2. Tubu kwa ajili ya nafasi uliyopo ambayo kuna mtu au watu walishawahi kukaa katika nafasi hiyo au wanahitaji nafasi hiyo,
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
Ngoja nikupe mfano hai
Mimi Mt Daudi Makubi kuna kipindi niliteuliwa kuwa shemasi wa Kanisa na mpaka sasa ni shemasi wa kanisa ninalo abudu,
Baada ya kupewa nafasi hiyo kwa muda mrefu nilipata ufunuo wa maombi ya toba kwa ajili ya nafasi yangu ya ushemasi, Kanisani hapo, nilitubu pia kwa ajili ya makosa ya walionitangulia ili nisitembee kwenye makosa yao (hata kama siyajui makosa yao hata moja)
Sasa kama Mimi nilipewa ufunuo wa kuombea kiti/nafasi ya cheo cha kikanisa vipi kwa wewe uliyechukua nafasi ya mtu serikalini, au taasisi kwenye kampuni n.k?
Vipi kwa wewe uliyechukua chumba cha biashara ambacho kilikuwa na mtu kabla yako,
Vipi wewe ambaye umechukua nafasi ya mtu aliyefukuzwa na ukapewe wewe,
Vipi kwa wewe ambaye umenunua ardhi ambayo wengine haikuwapa faida toka waimiliki mpaka wakaiacha au kukuuzia wewe ???
Ndugu, inakupasa kuwa muombaji na mtoaji sana ili upate baraka za MUNGU na ulinzi katika eneo hilo.
Kuna watu huota ndoto kila Mara wakiona nyoka maeneo yao ya kazi, ndugu yuko mtu alikuwa anaona nyoka kazini kwake kumbe yule nyoka ni jini ambaye hupewa kafara ili kulinda kiti, usipomtowesha kwa jina la YESU KRISTO atakusumbua sana na hata kukuharibia sana kazi yako.
Kuna mpaka shule au vyuo wamiliki walizika wanyama wa matambiko ili kuvuta watu kipepo lakini baada ya masomo ukitoka hapo hakuna kupata ajira ndugu yangu sio watu wote ni wema kwako, mwema kwako ni YESU KRISTO tu na watumishi wake waaminifu,
Sasa kama wewe ndio unasoma shule hiyo iliyofanyiwa uchawi unaweza ukatoka shuleni hapo umeshikiliwa na uchawi wa ardhi hiyo, ndio maana ni muhimu sana kuombea ardhi ya eneo unaloishi kwa muda au unaishi maisha ya kudumu ili utawale na kumiliki maana tumepewa kumiliki na kutawala.
3. Ombea ufahamu wako ili umtii ROHO MTAKATIFU ambaye ndiye mwalimu wa kweli wa kukupeleka kwenye mafanikio yako sahihi yaani usizitumie akili zako bali ROHO MTAKATIFU Atawale,
Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama." ROHO MTAKATIFU ndie mshauli wa kweli na msaidizi wetu.
4. Futa vifungo vya giza katika ardhi ya eneo lako la kufanikiwa kwako.
Kumbukumbum la torati 12:1-3" Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa BWANA, MUNGU wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi. Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."
5. Simamisha agano na MUNGU wako katika eneo hilo, kwa sadaka inayoambatanishwa na maombi ili kuondoa maagano ya kipepo yaliyofanyika hapo.
Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."
Ukisimamisha agano na MUNGU ujue maagano ya kishetani katika ardhi hiyo yataondoka,
Ombea pia sadaka zako na zaka zako unazozitoa kutokana na kazi yako eneo hilo.
6. Ita baraka ya MUNGU iambatane nawe
Isaya 58:9 "Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;"
7. Omba MUNGU akufunulie hazina za sirini ambazo ni baraka zako.
Isaya 45:3 "nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, MUNGU wa Israeli."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU, ila nina neno moja la mwisho kwako ndugu yangu mpendwa.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi na hii ni kweli kabisa na hakika.
Je, Umejiandaaje rafiki yangu ndugu yangu?
Je, Unaendeleza Dhambi ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU atakapo kuja? Je, Umeshika Wokovu na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama bado Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu usicheze cheze na dhambi.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha pia dunia na fahari zake zooote zitapita
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka na kudhani kuwa bado una muda hapana muda ni sasa.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako aliekulipia gharama ya DAMU yake pale msalabani ili tu akuweke huru.
Ni mimi ndugu yako Mt Daudi Makubi
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255 756 717 689
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu kama ulivyo ili uwafikie wengi asante na MUNGU akubariki.
Comments
Post a Comment